Wakazi waonywa dhidi ya utapeli Konyao

Na Benson Aswani,
Wakazi wa eneo la Konyao eneo bunge la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi wametahadharishwa dhidi ya kutapeliwa na baadhi ya watu wanaozunguka wakidai kuwasajili ili wafidiwe kuhusiana na vita vya ukoloni.
Kulingana na Rosana Kashiol, zaidi ya kina mama 100 tayari wamesajiliwa huku wakiwasilisha vitambulisho vyao vya kitaifa kulipia shilingi 600 katika zoezi hilo la usajili, ambapo hadi kufikia sasa waliowasilisha vitambulisho vyao hawajarejeshewa.
“Kuna watu wanawasajili kina mama huku eti kwa mambo ya vita ya maumau, kuna wale ambao wamejiandikisha kwa kulipa shilingi 600 na kupeana vitambulisho vyao. La ajabu ni kwamba hadi sasa hakuna mama hata mmoja ambaye amerejeshewa kitambulisho chake,” alisema Kashiol.
Kashiol alisema kwamba anayeendeleza zoezi hilo alidai kuwa shughuli hiyo imeidhinishwa na kamishina wa kaunti hiyo ya Pokot magharibi na hata kutoa stakabadhi zinazoidhinisha zoezi hilo na sahihi ya kamishina.
“Hawa watu wamesema kwamba wametoka kwa afisi ya kamishina wa kaunti hii. Walikuwa na makaratasi yenye yalikuwa na saini ya kamishina,” alisema.
Ni madai ambayo yalithibitishwa na naibu kamishina eneo la kacheliba Kenneth Kiprop, ambaye alikanusha taarifa za kuhusika afisi ya kamishina wa kaunti hiyo katika shughuli hiyo, akisema kwamba wametoa agizo la kukamatwa wanaoendeleza shughuli hiyo ya kuwatapeli wananchi.
Aliwataka wakazi kuwa makini na kutohadaiwa na watu wanaolenga kuwatapeli fedha zao.