WAKAZI WAHIMIZWA ‘KUTIA BREKI’ UZAZI KACHELIBA.

Wito umetolewa kwa wakazi eneo la Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi kukumbatia mpango uzazi kama njia moja ya kukuza kizazi chenye afya.

Ni wito wake naibu kamishina eneo hilo Kenneth Kiprop ambaye alisema kwamba raslimali zimeendelea kupungua ikilinganishwa na miaka ya awali na inafika wakati ambapo itakuwa vigumu kwa wazazi wenye idadi kubwa ya watoto kushughulikia familia zao.

Aidha Kiprop aliwasuta wanaume eneo hilo kwa kile alisema kuwaachia wake zao majukumu ya kushughulikia jamii, akiwataka kufahamu kwamba ndio walio na jukumu la kuhakikisha usalama wa jamii zao.

“Wale mnafanya hayo maneno ya kujenga dunia, tupunguze mwendo. Tupange familia zetu. Mali inapungua, si kama zamani. Halafu wanaume mwache tabia ya kuwaachia wake zenu majukumu ya kushughulikia jamii. Ni jukumu lenu kuhakikisha kwamba familia iko salama.” Alisema Kiprop.

Wakati uo huo Kiprop aliwataka kina mama wanaopata uja uzito eneo hilo kukumbatia huduma za kuzalia hospitalini akisema huduma ambazo zinatolewa katika vituo vya afya kabla ya kujifungua ni muhimu zaidi kwa afya ya mtoto.

“Nawahimiza pia kina mama ambao wanapata ujauzito kwamba hiyo ni baraka, na baraka unapasa kuitunza vyema. Tukumbatie huduma za hospitalini kwa sababu huduma hizo ni muhimu sana kuhakikisha afya ya mtoto ambaye umembeba.” Alisema.