Wakazi wahimizwa kukumbatia uhifadhi wa mazingira

Na Emmanuel Oyasi,
Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wamehimizwa kuhifadhi mazingira na kujizuia kukata miti kiholela ili kukabili changamoto ambazo zinatokana na mabadiliko ya tabia nchi.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shughuli ya upanzi wa miche katika msitu wa kamatira, mkewe gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin, Bi. Scovia Kachapin aliwahimiza wakazi kukumbatia zoezi la upanzi wa miti ili kuafikia malengo ya serikali ya upanzi wa miche bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

“Vile tunafahamu maono ya rais wetu ya kupanda miche bilioni 15 kufikia mwaka 2032, nawahimiza wakazi kuhifadhi misitu yetu. Tusikate miti ovyo. Na kama ni lazima, ukikata mti mmoja, unapanda miti miwili,” alisema Bi. Scovia.


Kauli yake imesisitizwa na afisa mkuu wa shirika la Keino sports events Martine Keino ambaye alielezea umuhimu wa msitu huo kwa jamii inayoishi karibu, kama vile chakula dawa za kiasili kando na historia inayozungumka msitu huo.


“Kuhifadhi mazingira ni kitu muhimu sana hasa msitu huu wa Kamatira ambao una historia muhimu. Pia tunapata kwamba misitu inatupa chakula, dawa za kienyeji pamoja na kukabili changamoto za mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Keino.


Kwa upande wake katibu wa shirika la kijamii la mazingira, Empowering Climate Actors Community based Organisation, Reuben Kimtai mmoja wadau wanaohakikisha msitu huo unatunzwa alisema watahikikisha uwepo wa miche ya kutosha ya kapanda kwenye msitu huo.


“Huu msitu una historia kubwa sana, na tuna nia ya kuhifadhi msitu huu kwa miaka mitatu ambayo tumepewa kuusimamia. Tutahakikisha kwamba kuna miche ya kutosha ya kupanda sehemu hii,” alisema Kimtai.