WAKAZI WA POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUTIA JUHUDI KATIKA SHUGHULI ZAO ZA KILA SIKU.
Wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuendelea kutia juhudi katika shughuli zao mbali mbali mwaka huu licha ya changamoto ambazo wamekumbana nazo mwaka jana.
Seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio amesema kuwa mwaka jana umekumbwa na changamoto tele kuu zaidi ikiwa janga la Corona ambalo lilipelekea kuathirika shughuli mbali mbali ikiwemo kalenda ya masomo huku akielezea matarajio kuwa mwaka huu utakuwa afueni kwa wakenya.
Aidha Poghisio amesema kuwa mwaka huu una shughuli nyingi ikiwemo uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa mwezi agosti hali ambayo itahitaji ushirikiano wa wakenya wote ili kutoa mazingira bora ya kuendelezwa shughuli za kawaida na kuimarishwa uchumi wa nchi.
Wakati uo huo Poghisio amesisitiza haja ya wakazi kudumisha amani hasa katika mipaka ya kaunti hii ya Pokot magharibi ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama, huku pia akiwataka wanasiasa kuendesha siasa za amani msimu huu wa siasa za uchaguzi mkuu ujao.