WAKAZI WA POKOT MAGHARIBI KUNUFAIKA NA UTEUZI WA MOJA KWA MOJA KUJIUNGA CHUO CHA KMTC.


Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi itaendelea kushirikiana kikamilifu na chuo cha mafunzo ya utabibu cha kapenguria KMTC ili kuhakikisha kuwa wanafunzi katika chuo hicho wanapata mafunzo ya viwango vinavyostahili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa madarasa katika chuo hicho, katibu wa kaunti John Karamunya amesema kuwa serikali inafungua vitengo mbali mbali katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria ili kutoa nafasi zaidi kwa wanafunzi kutoka chuo hicho kujifunza kuhusu taaluma yao ya utabibu kwenye hospitali hiyo.
Karamunya aliyemwakilisha gavana John Lonyangapuo ametoa wito kwa uongozi wa chuo hicho kuwapa angalau asilimia 30 ya wanafunzi kutoka kaunti hii ya pokot magharibi nafasi ya moja kwa moja ambapo hawatahitajika kutuma maombi ya kujiunga na chuo hicho kama wanafunzi kutoka nje ya kaunti hii.
Ni kauli ambazo zimesisitizwa na waziri wa afya katika kaunti hii Christine Apakoreng ambaye amesema lengo kuu la kufungua vitengo zaidi ni kuhakikisha wanafunzi hao wananufaika hata zaidi.
Kwa upande wake spika wa bunge la kaunti hii ya pokot magharibi Catherine mukenyang ameomba uongozi wa chuo hicho kutilia maanani wahadhiri wa chuo hicho kutoka kaunti hii ya pokot magharibi katika shughuli ya kupandishwa vyeo.
Afisa mkuu wa chuo hicho prof. Michael kiptoo amepongeza serikali ya kaunti kwa kukiunga mkono akiahidi ushirikiano mkamilifu wa chuo hicho na serikali ya kaunti kuhakikisha kinaimarika hata zaidi, huku akitoa hakikisho kuwa asilimia 30 ya nafasi katika chuo hicho zimetengewa wanafunzi wa kaunti hii ya pokot magharibi.