WAKAZI WA MOSESWO, KANGILKWAN WAKADIRIA HASARA YA MIFUGO KUFUATIA MKURUPUKO WA UGONJWA USIOJULIKANA.
Wakazi wa kijiji cha Moseswo, kangilkwan wadi ya mnagei eneo bunge la Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi wametoa wito kwa maafisa wa idara ya mifugo kufika eneo hilo kubaini kinachosababisha kufa kiholela mifugo wao.
Wakiongozwa na Yusuf Kachila wakazi hao walisema licha ya baadhi ya mifugo wao kutibiwa, visa vya ng’ombe kufa vimeendelea kuripotiwa katika kijiji hicho wakihofia huenda kuna mkurupuko wa ugonjwa wa mifugo ambao hawafahamu.
“Ng’ombe wanaugua kila wakati na kufa wakifuatana. Maafisa wa mifugo walifika huku wakatibu mifugo ila sasa tunaona hali inaendelea kuwa mbaya. Tunashuku huenda ni mkurupuko wa ugonjwa ambao hatufahamu. Tunaomba maafisa wa mifugo kufika na kupima sampuli za damu ili kubaini ni ugonjwa upi.” Alisema Kachila.
Aidha jamii moja eneo hilo ilidai kupoteza mifugo wao wote kufuatia ugonjwa huo, sasa wakisema kwamba hawana jinsi ya kujikimu kimaisha ikizingatiwa mifugo hao ndio waliokuwa tegemeo lao katika kufanikisha shughuli mbali mbali.
“Tumepoteza mifugo wetu wote kutokana na ugonjwa huu. Na mifugo hao ndio walikuwa tegemeo letu mbele na nyuma na sasa hatuna jinsi ambavyo tutashughulikia mahitaji yetu ya kila siku.” Walisema.