WAKAZI WA MASOL POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA MAKALI YA NJAA.
Na Emmanuel Oyasi.
Wakazi wa eneo la Masol Pokot ya kati kaunti ya Pokot magharibi wametoa wito kwa serikali kusambaza chakula cha msaada eneo hilo kutokana na hali kwamba wengi wa wakazi wanakabiliwa na baa la njaa.
Wakiongozwa na mwanaharakati wa haki za binadam Eric Kalikwon, wakazi hao walisema kwamba hali ya ukame imewaathiri pakubwa huku mifugo wao pia wakikosa lishe hali ambayo walisema imechangia swala la utovu wa usalama.
“Upande huu wa Masol kuna shida sana ya chakula. Watu wengi hawana chakula huku. Tunaomba serikali kuleta chakula cha msaada ili kuwasaidia watu wetu huku.” Walisema.
Wakazi hao walisema kwamba wanategemea mifugo kuwa uchumi wao na kutokana na hali ya ukame hawana jinsi ya kujiendeleza kwani mifugo wao wameathirika pakubwa.
“Kuna njaa kubwa sana huku kwa sababu ya ukame ambao umekithiri. Sisi hapa tunategemea mifugo kwa uchumi wetu na sasa wameathirika kwa sababu ya ukosefu wa lishe. Tunamwomba rais atusaidie sisi wakazi wa Masol.” Walisema.
Aidha wakazi hao walitaka kuimarishwa hali ya maafisa wa akiba NPR ili kuwapa nguvu ya kukabiliana na wahalifu.
“Tunaomba pia serikali kuwapa maafisa wa NPR pesa ili wapate motisha wa kutekeleza kazi yao ya kuleta usalama.” Walisema.