WAKAZI WA MAENEO YANAYOKUMBWA NA UTOVU WA USALAMA WAAGIZWA KUONDOKA AWAMU YA PILI YA OPARESHENI YA KIUSALAMA IKIANZA.
Wakazi wa eneo la Tukwel mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia tangazo la wizara ya maswala ya ndani ya nchi ambalo limewataka kuondoka mara moja eneo hilo kufuatia awamu ya pili ya oparesheni ya kiusama ambayo imeanza maeneo ambako kunashuhudiwa utovu wa usalama.
Kupitia gazeti rasmi la serikali, waziri wa usalama Kithure Kindiki aliorodhesha eneo la Turkwel miongoni mwa sehemu ambako kumetajwa kuwa hatari na ambako sasa vikosi vya usalama vinaelekeza juhudi za kuhakikisha majangili wanakabiliwa ipasavyo.
Kulingana na tangazo hilo, wakazi walipewa masaa 24 ambayo yalikamilika jumatatu saa mbili unusu, kuyahama maeneo hayo huku onyo ikitolewa kwa yeyote atakayepatikana maeneo hayo kwamba atachukuliwa kuwa mhalifu na kukabiliwa na vikosi vya usalama.
“Tumewaagiza wote wanaoishi maeneo yanayoripoti visa vya utovu wa usalama kuyahama maeneo hayo kufikia jumatatu saa mbili asubuhi. Mtu yeyote atakayepatikana maeneo hayo atachukuliwa kuwa jangili, au anayewasaidia majangili kutekeleza uhalifu, na atakabiliwa kama jangili.” Alisema Kindiki.
Hata hivyo wakazi wa eneo hilo na maeneo mengine ya kaunti hiyo wameisuta serikali kwa tangazo hilo wakisema kwa sasa hawana pa kuelekea na kwamba wakazi wengi sasa wanapitia hali ngumu ya maisha na kuwapa ilani ya muda mfupi kuwataka kuhama maeneo wanakoishi bila ya kuwatengea sehemu watakakoenda ni kuwahangaisha.
“Sisi ni wanadamu na hatuwezienda kama ndege. Watu watawezaje kutupa masaa 24 kuondoka na hatuna magari. Watu sasa hivi kaunti hii wanapitia hali ngumu ya maisha, na ilani kama hizi kutolewa wakati huu ni kutuhangaisha.” Walisema wakazi.