WAKAZI WA MAENEO YALIYOATHIRIKA NA UTOVU WA USALAMA WATAKIWA KUWAREJESHA WANAO SHULENI.
Naibu gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole amewataka wazazi wa wanafunzi katika shule ambazo zilifungwa kufuatia utovu wa usalama maeneo ya mipakani kuhakikisha kwamba wanao wanaenda shuleni shughuli za masomo zinaporejewa kuanzia jumatatu.
Komole aliwahakikishia wazazi kwamba usalama utaimarishwa katika shule hizo baada ya serikali kuwaajiri maafisa wa akiba NPR ambao jukumu lao kuu litakuwa kuhakikisha shule zinasalia salama dhidi ya mashambulizi ya wahalifu.
Aidha Komole aliwataka wazazi kutokuwa na hofu kuhusiana na chakula shuleni kwani tayari serikali imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha kutosha wanapoendelea na masomo yao shuleni.
“Nawahimiza wazazi wa maeneo ya mipakani ambako shule zilifungwa kutokana na utovu wa usalama kuwapeleka watoto wao shuleni kwani sasa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba kuna usalama wa kutosha.” Alisema Komole.
Kauli yake Komole inafuatia miito ya wakazi wa maeneo hayo kwa serikali kupitia idara ya usalama kuhakikisha kwamba hali ya usalama inaimarishwa hata zaidi ili kuwapa watoto wao mazingira bora ya kuendeleza elimu yao baada ya kuathirika kwa kipindi kirefu.
“Tunataka serikali kuhakikisha kwamba shule ziko salama. Hatutaki kuwapeleka watoto wetu shuleni katika mazingira ambayo yatahatarisha maisha yao.” Walisema.