WAKAZI WA KANYERUS WAPONGEZWA KWA KUKUMBATIA WITO WA UJENZI WA VYOO.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi ipo tayari kushirikiana na mashirika mbali mbali ambayo yanaendeleza miradi ya kuwanufaisha wakazi wa kaunti hiyo, ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kwa viwango vinavyostahili.

Akizungumza katika hafla ya kuwasherehekea wakazi wa eneo la Kanyerus eneo bunge la Kacheliba kwa kuitikia wito wa kujenga vyoo, naibu gavana Robert Komole aidha aliwahimiza wanaoendeleza miradi hiyo kuwahusisha viongozi katika kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa ujenzi wa vyoo hatua aliyosema itaafikia malengo kwa upesi.

“Serikali ya gavana Kachapin iko tayari kushirikiana na mashirika ambayo yanaendeleza miradi kaunti hii ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma zinazostahili. Pia naomba mashirika haya kushirikisha viongozi hasa inapohusu swala la kuhamasisha wananchi ili kuafikia malengo ikizingatiwa ushawishi wa viongozi hawa kwa wananchi.” Alisema Komole.

Kwa upande wake waziri wa ardhi, nyumba na mipangilio ya miji kaunti hiyo Esther Chelimo aliwahimiza wakazi wa eneo hilo kutumia vyoo ambavyo wamejenga ili kuepuka magonjwa ambayo hutokana na mazingira machafu.

“Tunawapongeza wakazi wa eneo hili kwa kuitikia mwito wa kujenga vyoo. Ninalowahimiza ni kwamba isiishie tu katika kujenga bali pia tuvitumie ili tuepuke magonjwa ambayo mara nyingi husababishwa na mazingira machafu.” Alisema Chelimo.

Kauli yake ilisisitizwa na naibu kamishina wa Kacheliba Kenneth Kiprop ambaye aidha alipongeza wafadhili wa mradi huo eneo hilo aliosema kwamba utawafaa zaidi wakazi hasa kuhusiana na swala la afya.

“Kama wakazi wa Kanyerus tunapongza sana shirika ambalo limefanikisha mradi huu wa ujenzi wa vyoo. Hatua hii ni muhimu sana hasa katika kuhakikisha kwamba hali ya afya ya wakazi wetu imeimarika.” Alisema Kiprop.

Wahudumu wa afya maeneo ya mashinani ambao wamekuwa wadau wakuu katika kufanikisha mpango huo kupitia kuwahamasisha wananchi, wamesema kwamba hatua hiyo imepelekea pakubwa kupungua kwa magonjwa miongoni mwa wakazi.