WAKAZI WA JAMII YA POKOT WATOA WITO KWA SERIKALI YA UGANDA KUWAHAKIKISHIA USALAMA KARITA.


Wakazi wa eneo la Karita mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda wametoa wito kwa serikali ya rais Yoweri Museven kuzidisha juhudi za kuhakikisha amani inadumishwa miongoni mwa jamii za Pokot na Karamojong zinazoishi eneo hilo.
Wakiongozwa na Solomon Tukei, wakazi hao kutoka jamii ya Pokot walisema kwamba licha ya jamii ya Pokot kusalimisha bunduki jinsi ilivyoamriwa na serikali, wameendelea kushuhudia mashambulizi kutoka kwa wavamizi ambao wamesababisha maafa ya wakazi na mifugo wengi kuibwa.
Aidha Tukei alilalamikia kile amedai kunyakuliwa ardhi iliyokuwa ikikaliwa na jamii ya Pokot na shirika la wanyamapori la UWA Ugandan Wildlife Authority akiitaka serikali ya rais Museveni kuwafidia kwa kuwapa ardhi nyingine.
“Sisi kama wapokot tulipeana bunduki jinsi ilivyoagiza serikali ya Museveni kwa sababu tulikuwa na imani kwamba serikali itatulinda. Ila hivi karibuni utovu wa usalama umezidi. Mifugo wetu wameibwa na watu wetu wengi kupoteza maisha yao.” Alisema Tukei.
Tukei alipendekeza kurejelewa mkataba wa Nabilatuk Resolution ambao amesema kwamba ulisababisha kuwepo amani wakati ulipopitishwa kutokana na adhabu kali uliyoweka kwa yeyote aliyetekeleza wizi wa mifugo kabla ya kuvurugwa.
“Kulikuwepo na mkataba wa amani wa Nabilatuk resolution ambao ulichangia pakubwa kumaliza uhasama kati ya wapokot na karamojong. Mkataba huo ulitoa adhabu kali kwa mtu ambaye angepatikana ameiba mifugo kwa sababu ulimtaka kulipia mara mbili ya mifugo ambayo ameiba. Ila wakati mktaba huo ulivurugwa hali ikawa mbaya hata zaidi.” Alisema.