WAKAZI WA AMUDAT WASHAURIWA KUTOHOFIA OPARESHENI YA KIUSALAMA INAYOENDESHWA ENEO HILO NA MAFISA WA POLISI.
Wakazi wa eneo la Amudat mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda wametakiwa kutokuwa na wasi wasi kufuatia oparesheni inayoendelea ya kuondoa silaha haramu katika mkoa wa karamoja.
Akizungumza na waandishi wa habari, RDC wa Amudat Betty Akelo alisema kwamba nia ya oparesheni hiyo ni kuondoa silaha miongoni mwa raia zinazomolikiwa kinyume cha sheria na wala haikusudii kuwahangaisha wakazi.
Alisema kwamba wale wanaokamatwa kimakosa na kupatikana bila hatia huachiliwa huru.
“Nataka wananchi wafahamu kwamba oparesheni hii hainuii kumhangaisha yeyote. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanapokonywa ili kuhakikisha usalama unadumishwa eneo hili.” Alisema Akelo.
Akelo aliwasihi wenyeji wa eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama kwa kuwatambua wahalifu wanaoishi miongoni mwao na kutowaficha ili kurahisisha shughuli hiyo na na wakati uo huo kusaidia katika kuimarisha usalama miongoni mwao.
“Nawahimiza wakazi kushirikiana kikamilifu na maafisa wa usalama. Wasiwatoroke polisi na kujificha vichakani. Wasiwafiche wahalifu pia bali wawatambue ili zoezi hili lifanikiwe.” Alisema.
Akelo alisema wamekuwa wakiwakumbusha maafisa wa usalama kuendesha shughuli hiyo kwa nidhamu na kujizuia dhidi ya kuwahangaisha raia, akiwahimiza wakazi kuwasilisha malalamishi kwa afisi yake iwapo watadhulumiwa kwa njia yoyote na maafisa wa polisi wanapoendeleza oparesheni hiyo.
“Tumekuwa tukiwakumbusha maafisa wetu kuhakikisha kwamba wanazingatia nidhamu ya hali ya juu wanapoetekeleza oparesheni hii. Na nawahimiza wananchi kufika katika afisi yangu na kuwaripoti maafisa watakaoendeleza dhuluma yoyote dhidi ya raia wakati wa zoezi hili.” Alisema.