WAKAZI TRANS NZOIA WATAKIWA KUJITOKEZA KUFANYIWA UCHUNGUZI WA MACHO.


Wito umetolewa kwa umma katika kaunti ya Trans nzoia kujitokeza na kufanyiwa uchunguzi wa macho ili kubaini iwapo wanakumbwa na matatizo yoyote mbali na kupata matibabu ya mapema.
Wakihutubu baada ya kuzuru hospitali kuu ya macho ya mjini Kitale, Katibu msimamizi Kaunti hiyo Fredric Sifuna na waziri wa afya Clare Wanyama wametoa wito kwa wazazi kuwafayia wanao uchunguzi wa macho kupitia kwa uvumbuzi wa PEEK wake Dkt Hillary Rono ili kujua mapema iwapo wanao wana matatizo ya macho.
Wamesema kwa siku mbili zilizopita hospitali hiyo ya macho imefanya uchunguzi na matibabu ya bure kwa zaidi ya wagonjwa 300 wa macho na upasuaji kwa wagonjwa 25.
Kwa upande wake Daktari mkuu wa macho Kaunti ya Trans Nzoia Dkt Hillary Rono na Rais wa Lions club tawi la Trans Nzoia Richard Kamau wamesema maadhimisho ya siku ya macho duniani ni kutathmini hatua zilizopigwa katika matibabu ya macho mbali na kutafakari masaibu wanayopitia watu wanaoishi na ulemavu wa macho wakitoa wito kwa walio na matatizo hayo kutembelea hospitali hiyo ya macho.