WAKAZI TRANS NZOIA WATAHADHARISHWA KUHUSU MATAPELI MSIMU HUU.


Kufuatia ongezeko la wizi wa mitandao Cyber Crime msimu huu wa krismasi na mwaka mpya, wito umetolewa kwa umma kuwa wangaalifu na kujiepusha na watu wanaowapigia simu kwa madai ya kuwasaidia kupata nafasi za ajira au kandarasi kwa mashirika mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizara za serikali.
Kwa mujibu wa mwathiriwa mmoja kutoka mjini Kitale matapeli hao walijaribu kumwibia baada ya kumhadaa kuwa walikuwa na uwezo wa kumsaidia kupata kandarasi ya kuuza maharagwe katika hospitali kuu ya Rufaa mjini Kitale.
Kwa sasa mwathiriwa huyo ametoa wito kwa umma kuwa waangalifu haswa msimu huu wa sherehe kutokana na matapeli hao ambao wanatumia rununu kuwahadaa kisha wanawaibia fedha zao, mbali na kuonya wafanyakazi dhidi ya kufichua siri za mashirika yao kwa watu wasiowajua.