Wakazi Siyoi wapunguziwa mahangaiko ya kutafuta maji

Mradi wa maji Siyoi, Picha/Benson Aswani

Na Emmanuel Oyasi,
Wakazi wa Siyoi kaunti ya Pokot magharibi wamepata afueni baada ya serikali ya kaunti kupitia wizara ya maji kuzindua mradi wa maji eneo hilo utakaowanufaisha zaidi ya wakazi 5000 ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata raslimali hiyo muhimu.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maji haya, afisa mkuu katika wizara ya maji, mazingira, mali asili na tabia nchi Leonard Kamsait alisema kwamba uzinduzi wa maji haya utasaidia pakubwa kupunguza maradhi ambayo yanasababishwa na maji chafu.


Aidha Kamsait alisema uwepo wa maji eneo hilo utawapunguzia gharama wakazi pamoja na wafanyibiashara ambao wamekuwa wakilazimika kugharamika zaidi kupata bidhaa hiyo muhimu kwani sasa watayapata kwa urahisi ikizingatiwa yatakuwepo kwa masaa 24.


“Hii ni hatua kubwa sana ya kuhakikisha kwamba watu wetu wanapata maji safi na kuwakinga dhidi ya magonjwa ambayo yanatokana na maji chafu. Pia maji haya yatawapunguzia wafanyibiashara gharama ya kununua maji kwa matumizi yao ya kila siku,” alisema Kamsait.


Ni hatua ambayo ilipongezwa pakubwa na wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Carolyne Chepkemoi ambao walisema wamehangaika kwa muda kwani wamekuwa wakilazima kwenda mwendo mrefu kutafuta maji ambayo hata hivyo yamekuwa tatizo kwa afya yao.


“Tunashukuru sana kwa mradi huu wa maji. Kwa muda sana tumekosa maji hapa Siyoi. Tumekuwa tukinywa maji chafu ambayo pia tunalazimika kutembea mwendo mrefu kuyapata,” alisema Chepkemoi.