WAKAZI SIGOR WATAKIWA KUTOKUBALI KUHADAIWA NA VIONGOZI WANAOLENGA KULETA UHASAMA MIONGONI MWAO.
Mbunge wa Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong amewasuta baadhi ya viongozi wa kisiasa kaunti hiyo ambao alidai kwamba wanaeneza propaganda ambazo huenda zikachochea uhasama miongoni mwa wananchi.
Lochakapong alidai kwamba mmoja wa viongozi wa kisiasa katika kaunti hiyo anaeneza madai ya uongo kwa wananchi katika eneo bunge lake la sigor kwamba kuna kiongozi ambaye amewasilisha majina ya wakazi kwa idara ya Ujasusi ili wafanyiwe uchunguzi na kukamatwa.
Lochakapong aliwataka wakazi wa eneo hilo kutokubali kuhadaiwa na viongozi wa aina hiyo ambao alisema nia yao ni kuleta migawanyiko miongoni mwa wananchi kwa malengo yao ya kisiasa, akisisitiza kwamba serikali ina mikakati na mbinu za kutafuta habari kuhusiana na hali na maswala ibuka nchini.
“Kuna kiongozi mmoja alifika eneo langu na kuanza kueneza propaganda kwa wananchi kwamba kiongozi mmoja amewasilisha majina ya wakazi kwa idara ya DCI ili wafanyiwe uchunguzi na kukamatwa. Hizi ni propaganda ambazo zinaweza kupelekea uhasama miongoni mwa wananchi na hata kusababisha wananchi kupigana.” Alisema Lochakapong.
Wakati uo huo Lochakapong alilalamikia kile alidai kwamba serikali inaendesha oparesheni ya kiusalama eneo la bonde la kerio kwa mapendeleo hasa baada ya maafisa wa akiba NPR katika kaunti jirani kukabidhiwa bunduki kuimarisha doria huku kaunti hiyo ikitelekezwa.
“Hapa nchini sisi sote ni sawa, na sheria inapasa kuwa sawa kwa kila mwananchi. Lakini sisi kaunti hii tunaona ni kama tumetengwa na serikali kwa sababu majirani zetu wote wamepewa maafisa wa NPR na kukabidhiwa bunduki lakini sisi imesalia tu ahadi ambayo serikali imekuwa ikitoa kila mara.” Alisema.