WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUWA MAKINI NA VYAMA WANAVYOUNGA MKONO.

Na Benson Aswani
Baadhi ya viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kusisitiza haja ya wakazi wa kaunti hii kuunga mkono vyama vya kitaifa ambavyo vitahakikisha wanakuwa serikalini na pia kuwapa sauti ya kuamua mustakabali wa taifa.
Wa hivi punde kutoa wito huo ni mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye amesema kuwa wakazi wa kaunti hii watanufaika pakubwa na nyadhifa mbali mbali katika serikali itakayobuniwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao iwapo watakuwa na makini kuhusu vyama watakavyounga mkono.
Wakati uo huo Lochakapong ambaye ni mwandani wa naibu rais William Ruto amekariri kauli ya Ruto kuwa kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao kitakuwa baina ya Ruto na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga.
Aidha Lochakapong ameelezea haja ya viongozi wa kisiasa katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuheshimu uamuzi wa viongozi wenzao kuunga mkono vyama mbali mbali akisema kuwa wao kama viongozi wana lengo la kuongoza wakazi katika njia ambayo itakuwa ya manufaa kwao.