WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUKUMBATIA ELIMU YA MTOTO WA KIKE.

Mtoto wa kike katika kaunti hii ya Pokot magharibi ataweza kufanya vyema zaidi katika mitihani ya kitaifa iwapo jamii itawekeza zaidi kwao na kujitenga na ukeketaji pamoja na ndoa za mapema.
Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya ELCK Chesta eneo la Pokot ya kati Patricia Nandi amesema shule hiyo ilifanya vyema katika mtihani wa KCSE mwaka 2021 licha ya changamoto ambazo mtoto wa kike anakumbana nazo ikiwemo kutelekezwa na jamii na shinikizo za ndoa za mapema.
Amewataka wazazi katika kaunti hii kubadilisha mawazo yao kuhusu mtoto wa kike na kumpa nafasi ya kusoma sawa na wenzao wa kiume ili pia waafikie ndoto zao maishani.
Wakati uo huo Nandi amekiri kuwepo na changamoto katika sera ya serikali ya asilimia 100 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa kwa darasa nane kujiunga na kidato cha kwanza ambapo wengi wanafunzi ambao wanaripoti shuleni wanafika bila karo na mahitaji mengine muhimu.