WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUKUMBATIA BIASHARA YA USHANGA KATIKA KUJIKIMU KIMAISHA.

Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi hasa kina mama kukumbatia biashara ya ushanga ambayo imetajwa kuwa yenye manufaa makubwa na ambayo itawasaidia katika kukimu mahitaji yao ya kila siku.

Afisa katika mradi wa Kenya big dream program Billy Otieno alisema kaunti ya Pokot magharibi ni moja ya kaunti ambazo mara nyingi hushuhudia ukame ambao huathiri shughuli za kilimo, akitaja ushanga kuwa suluhu kwa changamoto za kifedha ambazo zinakumba jamii.

“Mafunzo haya ya ushonaji wa ushanga ni muhimu sana kwa kina mama hasa katika kaunti hii ambayo ni moja kati ya kaunti kame ambapo mara nyingi ni vigumu kupanda mimea. Hivyo wakijihusisha na shughuli ya ushanga itawasaidia kujikimu kimaisha.” Alisema Otieno.

Kauli hii ilisisitizwa na Jane Mayani kutoka shirika la world vision ambaye anahusika na mafunzo ya jinsi ya kutengenza bidhaa za ushanga, na ambaye alitoa wito kwa serikali za kaunti na mashirika mengine ya kijamii kuwawezesha kina mama wanaohusika na shughuli ya ushanga ili kuimarisha mapato yao.

“Ninatoa wito kwa serikali za kaunti na mashirika mbali mbali ya kijamii kuwa karibu sana na kina mama hawa na kuwasaidia katika shughuli hii ili waweze kuimarisha mapato kutokana na ushanga.” Alisema Cheptoo.

Kina mama ambao walipokea mafunzo kutoka shirika hilo la World vision walielezea matumaini ya kuimarika soko ya bidhaa hizo za ushanga hasa baada ya shirika hilo kuwakutanisha na watu kutoka maeneo mbali mbali ya nchi.

“Mara nyingi tukishona ushanga hatuna pa kupeleka. Lakini sasa tunashukuru watu wa world vision kwa sababu ya mafunzo haya na wametukutanisha na watu kutoka maeneo mbali mbali hali itakayotusaidia kupata soko.” Walisema.