WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUFANYA KIPEU MBELE ELIMU YA MTOTO.


Taifa la Kenya linapojumuika na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mtoto wa kiafrika hii leo, wito umetolewa kwa wazazi katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuzingatia pakubwa elimu kwa ajili ya wanao.
Mwanachama wa kaundi la Lions katika kaunti hii ya pokot magharibi Carolyne Menach amesema kuwa kando na kuwa ni haki ya mtoto kupokea elimu kulingana na sheria za taifa la kenya, wazazi wanafaa kufahamu kuwa ni muhimu kwa wanao kupata elimu kwani itawasaidia katika siku za usoni.
Aidha Menach ametoa wito kwa wazazi kujitenga na tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji na ndoa za mapema, ili kumpa fursa mtoto wa kike kupata elimu na kufanikisha ndoto zake, huku pia akiwataka wadau kutia juhudi katika kukabili tamaduni hii miongoni mwa jamii.
Wakati uo huo menach ametoa wito kwa walio na uwezo katika jamii kuwasaidia watoto kutoka jamii masikini hasa walemavu ili kuwawezesha pia kujiona kuwa jamii inawajali.