WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUENDELEA KUJITOKEZA KUJISAJILI KUWA WAPIGA KURA.

Na Benson Aswani
Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameendelea kuwashinikiza wakazi hasa vijana walio na vitambulisho kujitokeza kwa wingi kujisajili kuwa wapiga kura katika zoezi la kuwasiliji wapiga kura wapya linaloendelezwa kote nchini na tume ya uchaguzi IEBC.
Kulingana na Poghisio ni kupitia tu idadi kubwa ya wakazi waliojisajili kuwa wapiga kura ndipo wagombea wengi wa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao watavutiwa kaunti hii hali ambayo itaipa sauti katika siasa za kitaifa hivyo kunufaika na miradi ya maendeleo.
Aidha Poghisio amewataka makamishina wa tume ya uchaguzi IEBC kubuni mbinu za kuwafikia wakazi hasa ambao ni wafugaji wa kuhamahama, ikiwemo kuwafuata maeneo ambako wamehamia na kuwasajili kuko huko na kutosubiri warejee maeneo yao ili kuafikia idadi kubwa ya wanaosajiliwa.
Wakati uo huo seneta Poghisio ametoa wito kwa vijana katika kaunti hii kutokubali kutumika na wanasiasa kuzua vurugu katika hafla mbali mbali za siasa na badala yake kudumisha amani hasa wakati huu ambapo uchaguzi mkuu wa mwaka ujao umekaribia.