WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUBADILI DHANA KUHUSU VYUO VYA KIUFUNDI NA KUVIKUMBATIA.

Wito umetolewa kwa jamii katika kaunti ya Pokot magharibi kubadili dhana kuhusu vyuo vya kiufundi vya TVET kuwa ni vya watu ambao walifeli kwenye mitihani yao.

Afisa wa mipango katika wakfu wa Zizi Afrique unaoendeleza uhamasisho kuhusu umuhimu wa kujiunga na vyuo hivyo Beria Wawira, alisema dhana hii imefanya vyuo vya TVET kusajili idadi ya chini zaidi ya wanaosomea kozi mbali mbali, akiwahimiza wananchi kuvikumbatia kwani ni kupitia vyuo hivyo ambapo watapata ujuzi wa kujiendeleza kimaisha.

“Kumekuwepo na dhana kwamba vyuo vya kiufundi ni vya watu ambao hawakufaulu masomoni, ila tunataka kubadilisha dhana hii. Watu wanapasa kujiunga na vyuo hivi ili kwamba wakaweze kupata ujuzi wa kujiendeleza kimaisha.” Alisema Wawira.

Ni wito ambao ulikaririwa na afisa katika shirika hilo Walter Odondi ambaye aidha alilalamikia ufadhili duni ambao vyuo hivyo vinapokea kutoka kwa serikali ikilinganishwa na unaotolewa kwa vyuo vikuu, akitaka serikali kuu na wafadhili wengine kuongeza ufadhili huo ili kuviwezesha kuwa katika nafasi ya kusajili wanafunzi wengi.

“Serikali imekuwa ikitenga mgao mchache sana kwa vyuo vya kiufundi ikilinganishwa na vyuo vikuu nchini. Hali hii imeathiri shughuli zake. Tunaitaka serikali kuongeza mgao huo ili vyuo hivi viweze kusajili wanafunzi zaidi kujiunga navyo.” Alisema Odondi.

Kwa upande wake waziri wa utumishi wa umma kaunti hiyo Martine Lotee alisema kwamba viwanda mbali mbali ambavyo vinajengwa kaunti hiyo vitahitaji vijana ambao wana ujuzi na itakuwa bora iwapo wakazi watakumbatia vyuo vya TVET na kupata ujuzi ili nafasi katika viwanda hivyo zisitwaliwe na watu kutoka kaunti zingine.

“Kuna viwanda ambavyo vinajengwa kaunti hii na viwanda hivi vitahitaji watu wa kufanya kazi. Itakuwa vibaya sana kwa viwanda hivi kuajiri watu kutoka nje ya kaunti hii huku wenyeji wakikosa ajira. Hivyo nawahimiza vijana kujiunga na vyuo vya kiufundi ili kupata ujuzi wa kuajiriwa katika viwanda hivi.” Alisema Lotee.