WAKAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUANZISHA NA KUSAJILI BIASHARA ZAO ILI KUNUFAIKA NA KANDARASI KUTOKA KWA SERIKALI.

Kampuni ya kuzalisha umeme KenGen inaendeleza uhamasisho kwa makundi ya vijana, wanawake pamoja na ya walemavu kuhusu jinsi ya kupata kandarasi za serikali zinazotolewa kwa makundi hayo kwa lengo la kuwaimarisha kiuchumi.

Akizungumza baada ya kuongoza mafunzo kwa makundi haya mjini Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi, meneja wa kampuni hiyo Anthony Kitungu alisema lengo kuu ni kuyawezesha kuwa katika nafasi ya kupata kandarasi walizotengewa, kampuni ya KenGen ikiwa imetenga nafasi maalum kwa ajili ya makundi haya.

“Kuna asilimia ya kandarasi ambazo zinatolewa na serikali kwa makundi ya vijana, kina mama na walemavu. Sisi kama KenGen tunaendeleza uhamasisho kwa wananchi maeneo mbali mbali kanda hii, ili kuwawezesha kuwa katika nafasi ya kupata kandarasi hizo.” Alisema Kitungu.

Chifu wa Kositei Asiwoi Afrikana alipongeza mafunzo hayo akitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo hasa vijana kutumia mfunzo ambayo wamepokea kutoka kampuni hiyo kujihusisha katika biashara na kusajili biashara zao ili kuwa katika nafasi bora ya kupata kandarasi kutoka kwa serikali.

“Nawaomba wakazi wa eneo hili hasa vijana kutumia mafunzo ambayo wamepewa kuanzisha biashara na kisha kuzisajili ili wawe katika nafasi ya kupata kandarasi za serikali na kujiimarisha kiuchumi.” Alisema Afrikana.

Kauli yake ilisisitizwa na baadhi ya wafanyibiashara ambao walihudhuria mafunzo hayo wakiongozwa na Brenda Juma ambao aidha waliwataka wakazi wa kaunti hii kutumia fursa hii ili kujiimarisha kiuchumi.

“Nawaomba wafanyibiashara wenzangu kwamba tutumie fursa hii ambayo tumepewa na serikali, tusajili biashara zetu ili tunufaike na kandarasi hizi.” Walisema.