WAKAZI POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA KUTOWAKILISHWA VYEMA KATIKA SERIKALI YA KENYA KWANZA.

Wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wametoa wito kwa rais William Ruto kuhakikisha kwamba kaunti hii inawakilishwa vyema katika serikali yake.

Wakiongozwa na Joseph Limasia mkazi wa eneo la Kacheliba, wakazi hao walisema kwamba kwa miaka mingi jamii ya Pokot imetengwa na serikali zilizotangulia hali ina wakazi ambao wana viwango hitajika vya elimu kushikilia nyadhifa mbali mbali serikalini.

Aidha walilalamikia hatua ya kuteuliwa mkazi mmoja pekee wa jamii ya Pokot kuhudumu katika serikali ya rais Ruto hali jamii zingine zimepewa  nyadhifa zaidi.

“Jamii ya Pokot imetengwa sana kwa miaka mingi kutokana na dhana kwamba wakazi kutoka jamii hii hawajasoma. Hivi majuzi ni mkazi mmoja tu ambaye ameteuliwa kuhudumu kama katibu wa wizara huku jamii zingine nchini zikitengewa nyadhifa nyingi serikalini.” Alisema Limasia.

Wakati uo huo Limasia alidai kwamba vijana wengi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamepoteza matumaini katika serikali ya rais Ruto kutokana na wengi wao kukosa ajira kinyume na alivyoahidi rais Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwezi agosti mwaka jana.

“Vijana wengi wa kaunti hii wamepoteza matumaini na serikali hii ya rais Ruto kwa sababu wengi wao hawana ajira licha ya rais Ruto kuwaahidi kuboresha maisha yao kwa kubuni nafasi za ajira kwa ajili yao wakati wa kampeni swala ambalo halijatimia hadi kufikia sasa.” Alisema.