WAKAZI POKOT MAGHARIBI WAHIMIZWA KUUNGA MKONO CHAMA CHA KANU.


Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ametoa wito kwa wakazi wa kaunti hii kuunga mkono kikamilifu chama cha KANU kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akizungumza baada ya chama hicho kumwidhinisha rasmi kinara wake Gideon Moi kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao, Poghisio amesema kuwa KANU ndicho chama imara na chenye mwelekeo huku akielezea matumaini kuwa kitaunda serikali ijayo.
Poghisio amesema kuwa licha ya kuwa KANU ni moja ya vyama tanzu vya muungano wa One Kenya Alliance ambapo utalazimika kuafikiana kuhusu mgombea atakayepeperusha bendera ya muungano huo, hatua ya Moi kuwa wa kwanza kutangaza rasmi azma ya kugombea kiti hicho inatoa uwezekano mkubwa kwake kuongoza muungano huo.