WAKAZI POKOT MAGHARIBI WAHIMIZWA KUCHANGIA JUHUDI ZA KUIMARISHA USAFI TAIFA LINAPOADHIMISHA WIKI YA USAFI.

Taifa likiadhimisha wiki ya usafi idara mbali mbali katika serikali ya kaunti hii ya Poikot magharibi zimeelezea kushirikiana kuhakikisha kwamba usafi wa mazingira unaimarishwa katika kaunti hii.

Akizungumza wakati wa kuzindua rasmi shughuli ya usafi mjini makutano, waziri wa afya kaunti hii Cleah Parklea aliwahimiza wakazi wa makutano na maeneo mengine katika kaunti hii kuhakikisha kuwa wanazingatia usafi maeneo wanakotekelezea shughuli zao.

“Tumekutana leo mjini Makutano kuzindua rasmi wiki ya usafi. Nawahimiza wakazi wa makutano na miji mingine katika kaunti hii kufanya mazoea usafi maeneo wanakotekelezewa shughuli zao ili kuhakikisha mazingira bora.” Alisema Parklea.

Waziri wa maji kaunti hii Laki litole ameelezea umuhimu wa kudumishwa usafi maeneo ya mijini akisema kuwa serikali yake itashirikiana kikamilifu na ile ya afya katika kuhakikisha usafi wa mazingira na hivyo kuimarisha afya ya wakazi.

“Sisi sote tunavyofahamu usafi ni muhimu kwa maisha yetu. Tusipofanya usafi ina maana kwamba mfumo wa kupitisha maji chafu utashikana na maji safi na hivyo kusababisha magonjwa kwa watu wetu. Wizara yangu itashirikiana kikamilifu na wizara ya afya kuhakikisha mazingira bora kwa watu wetu.” Alisema Litole.

Kwa upande wake Esther chelimo waziri wa ardhi na mipangilio ya miji, ameweka bayana kuwa wizara yake itahakikisha kwamba ujenzi wa majumba katika kaunti hii utazingatia utaratibu unaofaa na hata kuhakikisha sehemu za kutupa taka zinatengewa maeneo ambako haziwezi kuiathiri afya ya wananchi.

“Tunataka kuhakikisha kwamba ujenzi wa majumba katika miji ya kaunti hii unazingatia taratibu zilizopo, tupangilie miji yetu vizuri na kuhakikisha kwamba sehemu za kutupa taka na ujenzi wa vyoo zinawekwa maeneo salama.” Alisema Chelimo.