WAKAZI POKOT MAGHARIBI WAHAKIKISHA HUDUMA BORA ZA AFYA.

Mbunge wa sigor katika kaunti hii ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ameelezea imani kwamba sekta ya afya katika kaunti hii ambayo imetajwa kuwa na changamoto tele katika uongozi uliotangulia itaimarika chini ya uongozi wa gavana Simon Kachapin.

Akizungumza na wanahabari Lochakapong amewataka wakazi kuwa na imani na utawala wa gavana Kachapin anaosema kuwa utahakikisha hospitali na vituo vyote vya afya katika kaunti hii ya Pokot magharibi vinakuwa na dawa za kutosha.

Aidha Lochakapong amewahakikishia wakazi kwamba wao kama viongozi watajitwika jukumu la kusukuma na kuhakikisha kuwa sekta ya afya kwenye kaunti hii inaimarika pakubwa.

“Kulikuwa na tatizo la dawa kukosekana katika vituo vingi vya afya kaunti hii na tunafahamu kwamba swala hilo liko katika mipango ya gavana. Sisi kama viongozi tutasukuma kuhakikisha kwamba zahanati zote katika kaunti hii zinapata dawa za kutosha.” Alisema Lochakapong.

Wakati uo huo Lochakapong amesema kwamba hali katika hospitali ya Kapenguria itaimarishwa na kuboreshwa huduma ili kuzuia hali ambapo wakazi katika kaunti hii wanalazimika kutafuta huduma katika hospitali nje ya kaunti hii.

“Nafahamu kwamba hata hii hospitali ya Kapenguria kazi itafanyika ili iwe hospitali ya rufaa. Haina maana mtu kutoka maeneo ya Sigor, Cheptulel, Seker kufika Kapenguria halafu aambiwe aende hadi Eldoret.” Alisema.