WAKAZI POKOT MAGARIBI WAKANYWA DHIDI YA KUWAZIA KUJIUNGA NA MAANDAMANO YA AZIMIO.

Mbunge wa Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto amewataka wakazi wa kaunti hiyo kutojihusisha na maandamano ambayo yanaendelezwa maeneo mbali mbali ya nchi na vinara wa chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya.

Moroto alisema kwamba japo kinara wa muungano huo Raila Odinga amepigania mambo mengi humu nchini ambayo wakenya wanaendelea kufurahia ikiwemo serikali za magatuzi, anafaa kutumia njia bora ya kuwasilisha lalama zake kando na maandamanao ambayo amesema yanalemaza shughuli nyingi nchini.

“Nawahimiza watu wangu wa Kapenguria na hata pokot magharibi kwa jumla kujitenga na maandamano ambayo yanaendelezwa na muungano wa azimio. Ndio, tunaheshimu kazi ambayo imefanywa na Raila Odinga na wenzake ikiwemo ugatuzi ambao tunafurahia sasa.  Lakini ni wakati ambapo anafaa kutumia mbinu mbadala kupigania anayoshinikiza kando na maandamano.” Alisema Moroto.

Hata hivyo Moroto alionekana kutofautiana na viongozi wanaomsuta Raila kufuatia visa vya uporaji ambavyo vimeshuhudiwa hivi karibuni wakivihusisha na harakati za kiongozi huyo, akisema kwamba ni watu wenye nia potovu ambao wanatumia fursa ya maandamano kutekeleza uhalifu huo.

“Kuna wakora ambao wanapitia maandamano haya yanayostahili kuwa ya amani. Kuna watu ambao wanaandamana kwa halali kushinikiza mambo mbali mbali lakini sasa kuna wale ambao wanakuja na nia tofauti ya kupora mali. Kwa hivyo si kila mtu anayeandamana ni mporaji.” Alisema Moroto.