WAKAZI POKOT KASKAZINI WATAKIWA KUKUMBATIA UPANZI WA MITI.

Na Benson Aswani
Wakazi eneo la pokot kaskazini kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kukumbatia zoezi la upanzi wa miti ili kuafikia asilimia 10 ya misitu nchini.
Akizungumza na kituo hiki afisa wa misitu eneo la pokot kaskazini Daniel Nyakworo amesema kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa anapanda angalau miche miwili au mitano kila msimu wa mvua ili kuchangia juhudi za kuafikia kiwango hicho cha misitu.
Nyakworo amesema kuwa kwa sasa taifa limefikia asilimia 9 ya misitu na kuwa marufuku dhidi ya biashara ya uchomaji makaa yataondolewa tu na serikali iwapo lengo la asilimia kumi ya misitu kitaifa litaafikiwa.
Wakati uo huo Nyakworo amesema marufuku ya biashara ya makaa ingalipo na iwapo mtu angependa kukata mti ili kuchoma makaa kwa ajili ya kibiashara ni lazima atafute leseni kutoka kwa afisa wa misitu ambapo atakayepatikana akisafirisha makaa bila leseni atachukuliwa hatua.