WAKAZI MASOL WANUFAIKA NA MRADI WA UJUZI MANYATANI.
Zaidi ya wakazi 600 kutoka kaunti za wafugaji wamenufaika kutokana na mradi wa ujuzi manyatani ambao unatoa mafunzo ya kiufundi kwa wakazi katika kaunti hizi ili kuwapa uwezo wa kujiendeleza kimaisha.
Akizungumza eneo la Masol katika kaunti ya Pokot magharibi wakati wa kufuzu kwa kwa wakazi walioshiriki mafunzo haya, mshirikishi wa mradi huo ambao unafadhiliwa na shirika la USAID Peter Ngumo alisema mradi huo unalenga zaidi kaunti za wafugaji kutokana na idadi kubwa ya wakazi ambao hawajapata elimu.
“Tuko hapa leo kwa shughuli hii ya kufuzu vijana ambao wamekamilisha mafunzo yao katika mradi wa ujuzi manyatani. Tulianzisha mradi huu hasa katika kaunti za wafugaji kwa sababu hizi ni kaunti ambazo ziliachwa nyuma na hivyo wakazi wengi hawajapata masomo.” Alisema Ngumo.
Ni kauli ambayo ilitiliwa mkazo na mshirikishi wa shirika la NRT kaunti za pokot magharibi na Baringo, mshirika mkuu katika mradi huo Kadir Goru ambaye aidha alisema kwamba mafunzo haya ni muhimu kwa vijana maeneo haya kwani yatawapelekea kujihusisha na shughuli za kujipatia riziki na kujitenga na swala la wizi wa mifugo.
“Hizi ni kaunti ambazo zimekuwa zikishuhudia visa vingi vya utovu wa usalama na mradi huu wa ujuzi manyatani utawasaidia wengi kutafua shughuli ya kufanya kujipatia pato lao la kila siku na hivyo kujitenga na maswala ya wizi wa mifugo.” Alisema Goru.
Baadhi ya wakazi waliofuzu katika mradi huo walipongeza wadau waliofanikisha mafunzo hayo wakisema kwamba sasa wako katika nafasi bora ya kujiendeleza kimaisha kwa kutumia ujuzi waliopokea.
“Nashukuru NRT kwa mafunzo haya. Kwa sasa naweza kujifungulia biashara yangu na kujipatia riziki yangu ya kila siku na hivyo kuisaidia jamii yangu.” Alisema mmoja wa walionufaika.