WAKAZI MARIGAT WAKADIRIA HASARA KUFUATIA MAFURIKO YALIYOKUMBA MJI HUO WIKENDI.


Serikali ya kaunti ya Baringo imeahidi kuweka mikakati ya kudhibiti mafuriko kwenye eneo la marigat, eneo bunge la Baringo kusini baada ya mkasa wa jumamosi uliojiri kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.
Akiongea baada ya kuzuru eneo hilo, naibu gavana charles kipng’ok amesema tayari wamebuni kamati itakayotathmini hasara iliyosababishwa na mafuriko hayo na kutoa mapendekezo yake kuhusu jinsi ya kukabili hali sawia siku zijazo.
Kipngok hata hivyo ametaja ujenzi wa kiholela wa nyumba pamoja na mfumo mbaya wa kupitishia maji, kama baadhi ya sababu ambazo zilichangia mafuriko kushuhudiwa katika mji wa marigat.
“Hali hii imetokana na mfumo mbaya wa kupitisha maji taka na tumekuwa hapa na wahandisi ambao tume kubaliana kwamba hatua za haraka zinapasa kuchukuliwa katika kurekebisha mfumo huo.” Alisema.
Kauli yake imesisitizwa na mwakilishi wadi ya marigat Nickson Lemlem ambaye ameitaka serikali ya kaunti chini ya gavana Benjamin cheboi kuangazia jinsi itakavyoimarisha mikondo ya kupitishia maji taka.
“Serikali ya kaunti inapasa kulipa kipau mbele swala la mfumo wa kupitisha maji taka katika mji wa Marigat pamoja na mpangilio wa mji huu. Wananchi pia wanapasa kushirikiana kikamilifu na serikali ili kushughulikia hali hii haraka iwezekanavyo.” Alisema Lemlem.
Kwa upande wao waathiriwa wakiongozwa na ann chesire wamesema kuwa licha ya kusajili hasara baada ya bidhaa zao kuharibiwa na maji ya mafuriko, wanafuraha sababu hakuna maisha yaliyopotea.
“Maji yalisomba vitu vingi na hamna nyumba ambayo hayakuingia. Kila mtu hapa amepata hasara. Likini tunashukuru kwamba hakuna mtu aliyepoteza maisha kufuatia mafuriko hayo.” Walisema.
Ikumbukwe kwamba eneo la marigat hushuhudia mafuriko kila mwaka wakati wa mvua ya masika.