WAKAZI KONGELAI POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA MAISHA MAGUMU.
Wakazi wa eneo la kambi chafu eneo la Kongelai katika eneo bunge la Kapenguria kaunti hii ya pokot magharibi wamelalamikia hali ngumu ya maisha wanayopitia huku wakilaumu viongozi kwa kutochukua hatua zozote kuwaokoa na hali hii.
Wakiongozwa na Hellen Nasimiyu wakazi hao ambao wengi wao wanategemea ugemaji pombe ili kujikimu kimaisha wamedai watoto wao wanatumwa nyumbani kila mara kutafuta karo hali wameshindwa kuendeleza shughuli zao za kila siku kutokana na kuhangaishwa na maafisa wa polisi wanaotekeleza oparesheni za kila mara eneo hilo.
Wameelezea hofu kuwa wengi wa wanafunzi wameasi masomo kutokana na ukosefu wa karo na kuanza kujihusisha na michezo ya karata katika vyumba vya burudani hali ambayo imepelekea ongezeko la visa vya wizi na utovu wa usalama eneo hilo.
Aidha wakazi hao wamewalaumu viongozi katika kaunti hii kwa kutoa ahadi hewa kwa wakazi wa eneo hilo ambao wanakabiliwa na changamoto mbali mbali wakitolea mfano mkazi mmoja ambaye mifugo wake waliuliwa na radi na kuahidiwa msaada ambao hajaupokea hadi kufikia sasa.
Wakazi hao sasa wanatoa wito kwa viongozi wakiongozwa na gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi John Lonyangapuo, mwakilishi kina mama Lilian Tomitom pamoja na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto kuingilia kati na kuwatafutia suluhu ya mahangaiko wanayopitia.