Wakazi bonde la Kerio watakiwa kuwatambua wahalifu miongoni mwao

Na Benson Aswani,
Waziri wa usalama wa ndani kipchumba murkomen amewahimiza viongozi pamoja na wananchi kaskazini mwa bonde la ufa kushirikiana na vitengo vya usalama kama njia moja ya kumaliza uhalifu na wizi wa mifugo.
Akizungumza jumapili katika kanisa la katoliki eneo la Tapach kaunti ya Pokot Magharibi, Murkomen alisema ushirikiano huo utawawezesha maafisa wa usalama kuwanasa wahalifu ambao wanahangaisha Wakaazi.
Waziri Murkomen alisema kuwa idara ya usalama inalenga kufanya ukaguzi kwa maafisa wa akiba waliopewa majukumu ya kushika doria.
“Naomba wakazi wote wa bonde la Kerio, tushirikiane na vitengo vya usalama kwa kuwatambua wahalifu wote ambao wapo miongoni mwetu ili tuondoe uhalifu eneo hili,” alisema waziri Murkomen.
Aidha Murkomen alisema hivi karibuni wataweka mikakati dhabiti ya kuwanasa wahalifu akirejelea mauaji yaliyotekelezwa na wahalifu hao katika maeneo mbalimbali kaunti hiyo.
“Tumesema katika siku saba zilizo mbele yetu, lazima tutoe hawa na tuwalete wakamatwe na wapelekwe kotini. Na tumesema wale wote watakaokamatwa lazima wafikishwe mahakamani,” alisema.
Kauli ya Murkomen ilijiri huku makataa ya masaa 24 kwa wanaomiliki silaha kinyume na sheria katika eneo la bonde la kerio yakikamilika.
Naibu inspekta generali wa polisi Eliud Lagat alitoa makataa hayo siku ya jumamosi akiagiza wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzirejesha mara moja huku akiamrisha kuanza kwa oparesheni ya kuwatokomeza wahalifu wanaohujumu amani katika eneo hilo.
Pia mikutano ya kiusalama inayoendelezwa na wazee wa vijiji imefutiliwa mbali ili kutoa fursa kwa maafisa wa usalama kuendesha oparesheni za kiusalama kikamilifu katika eneo la Tot linalokabiliwa na visa vya wizi wa mifugo.
Ikumbukwe watu wanne wakiwemo wanafunzi wawili waliuliwa hivi majuzi katika visa viwili tofauti vya ujangili katika kaunti za Elgeyo Marakwet na Baringo.