WAKAAZI WAHAKIKISHIWA KUPATIKANA SULUHU KWA KIWANDA CHA SARUJI SEBIT POKOT MAGHARIBI

Wakazi wa eneo la batei katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamehakikishiwa kuwa kutapatikana suluhu kuhusu utata unaozingira kiwanda cha saruji cha sebit hasa kuhusiana na mbinu inayotumika kuwaajiri wanaofanya kazi katika kiwanda hicho.

Ni hakikisho lake mwakilishi wadi ya Batei Yusuf Long’iro ambaye alikuwa akizungumza baada ya kikao na machifu wa eneo hilo kuangazia malalamishi ya wakazi ambao wanadai kuwa uongozi wa kiwanda hicho unawaajiri wafanyikazi kutoka maeneo mengine licha ya ahadi kwamba wangepewa kipau mbele katika ajira.

Hata hivyo Long’iro ameelezea umuhimu wa kuwepo kiwanda hicho eneo hilo la Batei akisema kwamba kando na kuleta sura mpya, kitainua pakubwa uchumi wa wakazi wa eneo hilo kutokana na mazuri ambayo kitaandamana nayo.

Afisa wa uhusiano mwema katika kampuni hiyo ya Simba Cement Geofrey Sangote amesema kwamba mwanakandarasi anayeendeleza shughuli katika kiwanda hicho ana muda mfupi na ndiyo maana analazimika kutoa watu nje wenye ujuzi kutokana na hali kwamba wengi wa wakazi wa eneo hilo hawana ujuzi wa kazi hiyo ila akiwahakikishia kwamba swala hilo limeshughulikiwa.