WAKAAZI WA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WASHAURIWA KUTOA MAONI YAO KUHUSIANA NA MAREKEBISHO YA KATIBA KUPITIA BBI


Huku bunge la kaunti ya Pokot Magharibi likirejelea vikao vyake rasmi baada ya likizo ndefu ya janga la korona wakaazi wa kaunti hii wametakiwa kujitokeza katika maeneo tofauti kutoa maoni yao kuelekea mchakato wa kupasisha mswada wa marekebisho ya katiba ya mwaka wa 2020 kupitia ripoti ya maridhiano BBI.
Spika wa bunge la kaunti ya Pokot Magharibi Bi Catherine Mukenyang amesema zoezi la kutwaa maoni ya wananchi itaendelea katika maeneo bunge yote manne huku wawakilishi wadi wakizuru maeneo hayo kuzungumza na wananchi.
Mukenyang anasema bunge hilo litazingatia zaidi maoni yanayotolewa na wananchi kabla ya kuafikia uwamuzi wa kupasisha au kuangusha mswada huo.
Akizungumza na kituo hiki cha Kalya Radio, kiongozi wa wengi katika bunge hilo Thomas Amutang’orok amesema kikao chao cha kwanza kimehusisha suala la mchakato wa marekebisho ya katiba ya mwaka wa alfu mbili ishirini.
Amesema kamati maalum imebuniwa ili kuandaa vikao vingine vingi vitakavyowahusisha wakazi wa kaunti hii kwenye maeneobunge matano katika kaunti ya Pokot Magharibi ambapo raia watakuwa na uhuru wa kutoa maoni yao ya iwapo wanaiunga mkono ripoti yenyewe ama la.
Amutang’orok ametumia fursa hiyo kuipigia debe ripoti yenyewe akitaja kuwa na manufaa mengi hasa kwa kaunti ya Pokot Magharibi na magatuzi mengine ambayo yaliachwa nyuma kimaendeleo tangu taifa la Kenya lilipopata uhuru.