WAKAAZI WA KAUNTI HII POKOT WAHIMIZWA KUPANDA MITI ZAIDI

Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi kuendeleza juhudi za upanzi wa miti ili kuafikia asilimia kubwa ya misitu.

Akizungumza wakati wa upanzi wa miti katika shule ya upili ya wavulana ya Kapenguria kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuwakumbuka walioaga dunia kufuatia janga la corona, naibu kamishina kaunti hii ya Pokot magharibi Emily Ogola aidha ameelezea haja ya wadau husika kuendeleza uhamasisho kwa wakazi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu.

Ni kauli ambayo imesisitizwa na mshirikishi wa idara ya misitu kaunti hii Peter Kienze ambaye amesema kuwa wamekabiliwa na changamoto ya kutunza miche inayopandwa kufuatia uharibifu unaotekelezwa na mifugo, akiwataka wakazi kuhusika kikamilifu katika kuhifadhi misitu.

Meneja wa benki ya Equity tawi la Kapenguria ambaye ni mdhamini mkuu wa shughuli hiyo James Biwott amesema kuwa benki hiyo imekuwa ikiteleza shughuli ya upanzi wa miche kwa muda sasa na inanuia kufanya shughuli hiyo katika kaunti zote 47 nchini.