WAKAAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KURIPOTI KISA CHOCHOTE CHA DHULUMA DHIDI YA MTOTO MSICHANA

Na Benson Aswani
Jamii eneo bunge la Kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magharibi imeonywa dhidi ya kusalia kimya wakati wanaposhuhudia visa vya dhuluma dhidi ya mtoto wa kike badala yake wakihimizwa kuripoti kisa chochocte cha aina hiyo kwa idara husika.
Ni wito wake mwenyekiti wa shirika la vijana la Topoyo linaloshirikiana na DSW katika kukabili dhuluma za kijinsia eneo hilo Emmanuel Kudi ambaye amewataka wakazi kufika katika shirika hilo kuripoti visa hivyo ili kupata mwelekeo wa jinsi ambavyo waathiriwa wataweza kupata haki.
Kudi aidha ametoa wito kwa jamii kujitenga na tamaduni zilizopitwa na wakati ambazo amezitaja kuwa zinazokwenda kinyume na haki za mtoto wa kike akisema ni muhimu kwa sasa kila mmoja kukumbatia mwelekeo wa karne ya sasa.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na katibu wa shirika hilo Joseph Sarij ambaye amesema visa hivi vimechangia idadi kubwa ya watoto wa kike kuacha masomo huku akitoa wito kwa wazazi kuzingatia umuhimu wa masomo kwa wanao kwa manufaa yao ya baadaye.