WAKAAZI KAUNTI YA TRANSNZOIA WANAMTAKA GAVANA KUWATEUA MAAFISA WAADILIFU

Chama cha kutetea maslahi ya wafanyikazi katika kaunti ya Trans nzoia kimemtaka gavana wa kaunti hiyo George Natembeya kuwateua maafisa waadilifu na ambao wataimarisha utendakazi katika serikali yake anapotarajiwa kutangaza baraza lake la mawaziri.

Mwenyekiti wa chama hicho Samwel Kiboi amesema kwamba ni wakati mazingira ya wafanyikazi katika kaunti hiyo yanapasa kuimarishwa kupitia uteuzi wa mawaziri ambao wako tayari kuwajibika akidai wafanyikazi katika kaunti hiyo wamepitia wakati mgumu katika serikali iliyotangulia.

Wakati uo huo Kiboi amemtaka gavana wa kaunti hiyo George Natembeya kukaza kamba dhidi ya jinamizi la ufisadi akidai kwamba fedha nyingi za mlipa ushuru zilifujwa pakubwa katika uongozi wa serikali iliyotangulia katika kaunti hiyo.