WAKAAZI KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUZINGATIA USAWA MIONGONI MWA WATOTO WA KIKE NA KIUME


Na Benson Aswani
Jamii katika kaunti hii ya Pokot magharibi imetakiwa kuzingatia usawa miongoni mwa watoto wa kiume na wale wa kike.
Akizungumza katika hafla ya kuhamasisha umma dhidi ya dhuluma za kijinsia iliyoandaliwa katika shule ya upili ya Murpus, mwenyekiti wa mtandao wa kuwalinda watoto child protection network kaunti hii Carolyne Menach amesema kuwa mtoto wa kike ametelekezwa pakubwa na jamii.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na mkurugenzi wa idara ya watoto kaunti hii Philip Wepopa ambaye aidha amewahimiza wazazi kujitenga na hulka ya kuwaoza watoto wao mapema na badala yake kuhakikisha kuwa wanapata elimu kwa manufaa yao ya baadaye.
Kwa upande wake mkurugenzi wa elimu eneo la Kipkomo Evans Onyancha amewahimiza watoto wa kike kuwa na hekima, kutumia vyema muda wao na kuzingatia pakubwa masomo kauli ambayo imetiliwa mkazo na mwenyekiti wa shirikisho la walimu wakuu wa shule za upili KESSHA Consolata Sortum.