WAHUDUMU WA BODA BODA WATANGAZA KIVUMBI MNAGEI.


Wito umetolewa kwa wahudumu wa boda boda katika kaunti hii ya Pokot magharibi kudumisha amani na kutokubali kutumika na wanasiasa kuvuruga amani hasa msimu huu ambapo siasa za uchaguzi mkuu wa mwezi agosti zimeshika kasi.
Ni wito wake mwenyekiti wa wahudumu hao eneo bunge la Kapenguria Laban Ruto ambaye amesema kuwa kwa muda mrefu wahudumu hao wamekuwa wakitumika visivyo na wanasiasa na kisha kutelekezwa baada ya kukamilika msimu wa uchaguzi.
Ruto ambaye ametangaza nia ya kugombea kiti cha mwakilishi wadi ya Mnagei amesema kuwa ni wakati eneo hili linapasa kumpata kiongozi ambaye atawakilisha kikamilifu maswala ambayo yanakumba sekta ya boda boda kwani sekta hiyo imekumbwa na changamoto tele kutokana na kukosa mwakilishi wao katika uongozi wa taifa.
Ni hatua ambayo imeungwa mkono na wahudumu hao wakiongozwa na naibu mwenyekiti Moses Kemoi ambao wamesema kuwa ni kupitia mmoja wao kuwa katika bunge la kaunti ndipo matakwa yao yataweza kuangaziwa kikamilifu.