WAHUDUMU WA BODA BODA TRANS NZOIA WATISHIA KUTOLIPA USHURU KUFUATIA AHADI ZA ‘UONGO’ ZA GAVANA KHAEMBA.


Wahudumu wa boda boda katika Kaunti ya Trans Nzoia wametishia kutolipa ushuru na vile vile kufanya maandamano juma lijalo kutokana na kile wamedai ahadi za uongo za Gavana Patrick Khaemba alizotoa mwaka 2017 alipokuwa akitafuta kura huku wakielezea kujutia kutumiwa vibaya na Serikali hiyo.
Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa muungano wa Boda boda Kaunti ya Trans Nzoia James Nyakangi wahudumu hao wamemsuta Gavana Khaemba kwa kufeli kutimiza a hadi alizowapa kama vile mikopo.
Aidha Nyakangi ameshutumu Serikali hiyo kwa kuwaajiri wafanyikazi kutoka nje ya kaunti hiyo huku wahudumu wa Boda boda walioajiriwa kama Askari wa Mji wakifutwa kazi waliyokuwa wakifanya bila malipo kauli iliyoungwa mkono na Naibu Mwenyekiti wa muungano huo Tobias Bushuru ambaye ameitaka Serikali hiyo kuwarejesha wenzao kazini.
Wahudumu hao walifunga lango kuu la kuingia kwa afisi ya Gavana ya Patrick Khaemba hali hiyo ikiwalazimu askari wa kupambana na fujo kuingia ili kuwatawanya na kuruhusu wafanyikazi waliokuwa wamefungiwa nje kuingia ili kuwahudumia wananchi.