WAGONJWA WA FIGO WANAOSAKA HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA KAPENGURIA WALALAMIKIA HUDUMA DUNI


Wagonjwa wanaotafuta huduma za matatizo ya figo katika hospitali ya Kapenguria kaunti hii ya Pokot Magharibi wamelalamikia huduma duni katika kitengo hicho.
Wakiongozwa na Lucy Lotee wakazi hao wamesema huduma katika kitengo hicho zimeathirika pakubwa kutokana na ukosefu wa chakula kwa wagonjwa na wahudumu wa afya wanaowahudumia wagonjwa hao.

Inaarifiwa mkazi aliyepewa kandarasi ya kusambaza chakula katika hospitali hiyo alisitisha huduma hiyo tarehe mosi mwezi huu kutokana na hali kuwa hajalipwa kwa miezi sita kwa huduma alizotoa katika kipindi hicho.
Lotee sasa anatoa wito kwa serikali ya kaunti hii kupitia idara ya afya kumlipa mwanakandarasi huyo ili kurejesha huduma hiyo muhimu.
Juhudi za kupata kauli kutoka maafisa wa idara ya afya kaunti hii hazikuzaa matunda baada ya wizara hiyo kudinda kuzungumzia swala hilo.