WAGOMBEA WA UDA POKOT MAGHARIBI WAKABIDHIWA TIKETI.
Wagombea viti mbali mbali vya kisiasa katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kujipigia debe kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi agosti mwaka huu.
Wakizungumza katika makao makuu ya chama cha UDA jijini Nairobi baada ya kupokezwa rasmi vyeti vya kuwania nyadhifa mbali mbali, viongozi hao wakiongozwa na mgombea ugavana kaunti hii Simon Kachapin wamesema kuwa wakazi kaunti hii wamesalia katika hali ya umasikini kutokana na hali kuwa viongozi hawajatambua na kutumia raslimali zilizopo.
Kwa upande wake mwakilishi kina mama kaunti hii ya Pokot magharibi Lilian Tomitom ambaye anatetea wadhifa huo amewapongeza walioshinda mchujo wa UDA kaunti hii huku akiwahimiza wale ambao hawakufaulu kuchaguliwa katika mchujo huo kuendelea kuunga mkono chama na kutohadaiwa kughura chama hicho na vyama vingine.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na Mark Lumnokol anayetetea kiti chake cha eneo bunge la Kacheliba na ambaye amesema maandalizi ya zoezi la mchujo kaunti hii yalidhihirisha ukomavu wa demokrasia nchini huku akipuuza madai ya UDA kutokuwa na umaarufu kwenye kaunti hii.