WAGOMBEA NYADHIFA ZA KISIASA WAONYWA DHIDI YA KUVURUGA AMANI.


Idara ya polisi katika kaunti ya Pokot magharibi imetoa wito kwa wagombea nyadhifa mbali mbali za siasa katika uchaguzi mkuu ujao kaunti hii kuhakikisha kwamba wanadumisha amani wakati wanapoendeleza kampeni zao.
Akizungumza na kituo hiki kamanda wa polisi kaunti hii Peter Katam amewataka wanasiasa kujizuia na hali ambapo wanatofautiana kisera na kusababisha fujo na badala yake kila mmoja kuuza sera zake kwa amani ili kuandaa mazingira ya amani kwa ajili ya uchaguzi wa mwezi agosti.
Aidha Katam amewataka wagombea wote kuwasilisha kwa polisi ratiba ya kampeni zao na sehemu wanakotarajia kuendeleza kampeni hizo siku tatu kabla, ili kutoa nafasi kwa maafisa wa polisi kuhakikisha usalama katika kampeni zao.
Wakati uo huo Katam amewataka wagombea wote kuhakikisha kwamba wanakamilisha kampeni zao kufikia saa kumi na mbili unusu jioni akionya hatua kali kuchukuliwa dhidi ya atakayeendeleza kampeni baada ya wakati huo.