WAGOMBEA NYADHIFA ZA KISIASA WAONYWA DHIDI YA KUCHOCHEA WANANCHI.


Mgombea ugavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi kwa tiketi ya chama cha UDA Simon Kachapin amewataka wanasiasa wote wanaowania nyadhifa za uongozi kaunti hii kuendesha kampeni zao kwa njia ya amani na kutojihusisha na vurugu.
Kachapin amewataka wagombea wote kuwa makini na maneneo wanayosema wanapoendeleza kampeni zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti ili kujizuia na matamshi ya uchochezi ambayo huenda yakapelekea kuvurugwa amani.
Aidha Kachapin ambaye ni gavana wa kwanza wa kaunti hii amemsuta vikali kiongozi mmoja katika kaunti hii kwa kile amedai kueneza chuki kwenye mitandao ya kijamii akimtaka kuomba msamaha kwa kuwachochea vijana kushiriki vurugu.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na afisa wa uchaguzi wa tume ya uchaguzi ya IEBC kaunti hii ya Pokot Magharibi Joyce Wamalwa ambaye ameonya kuwa mgombea yeyote atakayepatikana akienda kinyume na sheria za uchaguzi kwa kuwachochea wananchi atachukuliwa hatua kisheria.