WAFUGAJI WATAKIWA KUPANDA CHAKULA CHA MIFUGO KWA WINGI MSIMU HUU WA MVUA.

Wafugaji katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kutumia msimu huu wa mvua kupanda kwa wingi chakula cha mifugo ili kuwa na uhakikisho wa lishe ya mifugo wakati mvua ikipungua.

Akizungumza baada ya kikao cha wadau mbali mbali kuangazia shughuli za kilimo kaunti hiyo msimu huu ambapo mvua inaendelea kushuhudiwa, mkurugenzi wa uzalishaji wa mifugo Paul Ruchong’ar alisema kando na kupanda nyasi wakazi pia wanafaa kutumia kipindi hiki kupanda aina fulani ya miti ambayo hutumika kama lishe kwa mifugo.

Wakati uo huo Ruchong’ar aliwahimiza wafugaji kuwa makini na mazingira ambapo wanakaa mifugo hasa kipindi hiki ambapo hushuhudiwa magonjwa mengi ya mifugo, kwa kuhakikisha kwamba wanakaa katika mazingira safi ili kuimarisha afya yao.

“Ni wakati wafugaji wanafaa  kuanza kupanda chakula cha mifugo kwa sababu mvua huja na kupotea. Na wakati ikienda tunafaa kuwa na chakula cha kutosha cha mifugo. Wafugaji watumie mvua inayoshuhudiwa sasa kupanda nyasi na aina ya miti ambayo hutumika kama lishe kwa mifugo.” Alisema Ruchong’ar.

Kwa upande wake mkurugenzi wa mamlaka ya kushughulikia majanga kaunti hiyo Joshua Mayeku alisema kwamba kikao hicho kilinuia kuwawezesha wadau katika sekta mbali mbali kuimarisha sekta zao kwa manufaa ya wakazi wa kaunti hii.

“Kikao hiki kimeleta pamoja wadau katika sekta mbali mbali ambapo kimetumika kuangazia jinsi ya kuimarisha sehemu zao za utendakazi kwa manufaa ya wakazi wa kaunti hii. Tunalenga kutumia yale ambayo yamejadiliwa hapa kuimarisha maisha ya wakazi.” Alisema Mayeku.