WAFUGAJI WA KUHAMAHAMA WATARAJIWA KUNUFAIKA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI.


Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na shirika moja la ujerumani la GIZ inanuia kutekeleza miradi kadhaa ya kuwanufaisha wakazi wa kaunti hasa wafugaji wa kuhamahama.
Akizungumza baada ya kuandaa kikao na maafisa wa shirika hilo ambao wamezuru kaunti ya Pokot magharibi mkurugenzi wa uzalishaji wa mifugo kaunti hii Paul Ruchong’at amesema kuwa serikali ya kaunti kwa ushirikiano na shirika hilo inalenga kujenga miundo mbinu katika barabara zinazotumika zaidi na wafugaji hao ili kuwafaa wakati wanapohama kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na mkurugenzi katika idara ya majanga na hali za dharura kaunti hii ya Pokot magharibi Raymond Sikamoi ambaye amesema kuwa mpango huo unanuia kuwawezesha zaidi wakazi hasa wafugaji na kuwarahisishia safari zao za kutafuta lishe kwa mifugo yao.
Wamesema kuwa maafisa hao watarejea kaunti hii juma lijalo na kuzuru maeneo mbali mbali kubaini miradi inayohitajika huku wakitoa wito kwa wakazi kushirikiana nao kwa kuwapa habari wanazohitaji ili kufanikisha miradi hiyo.