WAFUGAJI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUTII AGIZO LA KUSITISHA MASOKO YA MIFUGO KWA MUDA.
Waziri wa kilimo na mifugo kaunti ya Pokot magharibi Wilfred Longronyang ametoa wito kwa wakulima wa mifugoi katika kaunti hiyo kutii agizo la kusitisha shughuli ya kupeleka mifugo kwa soko kwa muda ili kushughulikia ugonjwa wa migiuu na midomo ambao umeripotiwa kukithiri baadhi ya maeneo ya kaunti hiyo.
Akizungumza baada ya kuongoza shughuli ya kutoa chanjo kwa mifugo dhidi ya ugonjwa huo eneo la Chepareria, Longronyang alisema kwamba ni kupitia hatua hiyo tu ambapo ugonjwa huo utakabiliwa kwani itakuwa vigumu kuumaliza iwapo mifugo watakuwa wakitangamana sokoni kutoka maeneo tofauti.
“Tumesimamisha masoko ya mifugo ili huu ugonjwa uishe ndipo turejelee shughuli kama kawaida. Na nawaomba wafugaji kuzingatia agizo hilo kwa sababu iwapo tutaruhusu mifugo kutangamana kila siku ya soko basi itakuwa vigumu kuumaliza.” Alisema Longronyang.
Wakati uo huo Longronyang aliwataka wanasiasa na wakazi kutoingiza siasa katika shughuli hiyo inayoendelezwa na serikali akisema lengo kuu ni kuhakikisha kwamba inawalinda wafugaji dhidi ya hasara ambayo inaweza kusababishwa na ugonjwa huo.
“Watu wasiingize siasa kwa shughuli hii ya kutoa chanjo kwa mifugo. Nimewasikia watu wengine wakieneza propaganda kuhusu chanjo. Lengo letu sisi ni kuhakikisha kwamba mifugo ya wakulima inasalia salama na hatungetaka mkulima yeyote apate hasara ambayo huenda ikasababishwa na ugonjwa huu.” Alisema.
Kwa upande wao wakulima walipongeza hatua hiyo na kutoa wito kwa serikali kuiwezesha zaidi wizara ya kilimo ili iwe katika nafasi ya kutekeleza shughuli hiyo bila ya changamoto ambazo zinashuhudiwa katika utoaji wa chanjo hiyo.