WAFANYIKAZI WA MRADI WA MAJI WA SIYOI-MURUNY WALALAMIKIA KUTOLIPWA KWA ZAIDI YA MWAKA MMOJA.

Wafanyakazi katika Mradi wa Kusambaza maji wa Siyoi – Muruny wameandamana wakilalamikia kutolipwa mishahara yao ya takriban milioni kumi.

Wafanyakazi hao walisema wamepitia changamoto kubwa tangu mradi huo ulipoanzishwa huku mwanakandarasi katika mradi huo akikosa kuwalipa pesa zao za mwaka mmoja sasa.

Itakumbukwa kwamba mradi huo ulianzishwa mwaka 2015 na rais mustaafu Uhuru Kenyatta, kabla ya kukwama kutokana na kucheleweshwa kwa pesa kutoka serikali kuu.

Hata hivyo aliyekuwa Mshirikishi wa utawala eneo la Bonde la Ufa George Natembeya aliutembelea mradi huo na kumwamuru mwanakandarasi huyo kuendeleza kazi yake.

“Tumefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja hapa na hatujawahi lipwa. Tumeumia sana kwa muda na sasa tunataka kulipwa pesa zetu. Hadi kufikia sasa tunadai mwanakandarasi huyu shilingi milioni 10.5.” walisema wafanyikazi.

Wafanyikazi hao sasa wanatoa wito kwa rais William Ruto kuingilia kati kuhakikisha kwamba wanalipwa fedha zao pamoja na kuhakikisha mradi huo unakamilika ili kuwanufaisha wakazi  zaidi ya laki tatu wanaolengwa.

“Tunatoa wito kwa rais aingilie kati na kuangazia mradi huu. Ahakikishe kwamba mwanakandsarasi huyu anatulipa pesa zetu na pia kukamilisha mradi huu ili wakazi wanaolengwa wanufaike na maji.” Walisema.