WAFANYIKAZI WA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WANAOHUDUMU KWA KANDARASI WALALAMIKIA KUFUTWA KAZI.
Baadhi ya wafanyikazi katika kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kile wamedai kufutwa kazi na serikali ya kaunti kupitia bodi ya huduma kwa umma wakihusisha hali hiyo na njama za kisiasa.
Wafanyikazi hao walisema kwamba licha ya kupitia hatua zote zinazohitajika kabla ya kuajiriwa wamepokezwa barua za kuwaachisha kazi kutoka kwa serikali ya kaunti huku wakilalamikia kutolipwa mishahara yao tangu mwezi aprili mwaka uliopita.
“Tumesikitishwa sana na hatua ya serikali ya kaunti kutufuta kazi hasa wale ambao tunafanya kazi kwa kandarasi tulioajiriwa mwaka jana. Tunashangazwa na hatua hii licha ya kwamba tulipitia taratibu zinazostahili kabla ya kuajiriwa. Hatujalipwa mshahara wetu tangu mwezi aprili mwaka jana.” Walisema wafanyikazi hao.
Wafanyikazi hao walidai kuwa huenda hii ni njama iliyopangwa kisiasa ili kupisha nafasi ya kuwaajiriwa wafanyikazi wapya ambao waliiunga mkono serikali iliyopo kwa sasa wakitoa wito kwa viongozi katika kaunti hii kuingilia kati na kutetea haki yao.
“Tunaona hii ikiwa mipango ya serikali ya kaunti kutaka kuwaajiri watu wengine ambao wanaona kwamba wanaunga mkono mrengo wao. Tunawaomba viongozi wote katika kaunti hii kuingilia kati na kuangazia swala hili ili nasi tupate haki yetu.” Walisema.
Ikumbukwe awali gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin alipinga vikali madai ya kuwafuta wafanyikazi hao walioajiriwa na serikali ya aliyekuwa gavana John Lonyangapuo akisema kwamba kandarasi yao ya kuhudumu ilikuwa imekamilika.
“Hamna mtu yeyote ambaye amefutwa kazi. Wafanyikazi wa kaunti ambao wanahudumu kwa kandarasi huwa wanabadilishwa au kuongezewa siku za kuhudumu. Na wanasaini kandarasi nyingine baada ya miezi mitatu kwa hivyo wale ambao wanaondoka wanafanya hivyo baada ya kipindi chao cha kuhudumu kukamilika.” Alisema Kachapin.